Kamati ya Kilimo kutafuta maoni ya wananchi kuhusu Mswaada wa Kahawa wa Mwaka wa 2021.
Kamati ya Kilimo na Mifugo katika Bunge la Kitaifa likiongozwa na Bw. mwenyekiti wake, Mbunge wa eneo bunge la Moiben Mh. Silus Tiren, imeanzisha ziara zake zilizoratibiwa kuhamasisha wakulima wa kahawa nchini kuhusu Mswada wa kahawa wa mwaka wa 2021.
Wabunge wanatarajiwa kuhusisha washikadao na wananchi kwa jumla katika kutengeneza sheria yoyote ile.
Kamati hiyo ya Kilimo na Mifugo ilianza mkutano wake kwa Kutembelea Ofisi ya Kamishna wa Kaunti ya Kiambu kama ilivyo desturi ya kamati za bunge zinapofanya ziara.
Hapo, Bw. Mwenyekiti Mh. Silas Tiren (Moiben) aliyeongoza kikao hicho alieleza kuwa kamati hiyo imejigawa majopo mawili; yeye akiongoza jopo la kwanza ambalo litazuru kaunti za Kiambu, Machakos, Embu na Kirinyaga.
Huku naibu wake Mh. Catherine Waruguru (Laikipia) akiongoza jopo la pili ambalo litazuru kaunti za Nandi, Kericho, Trans Nzoia na Bungoma.
Mswada wa kahawa(2021) unapania kudhibiti na kuendeleza ukuzaji wa sekta ya kahawa humu Nchini; kuanzisha chuo cha utafiti wa kahawa Nchini ambacho kitatengeza mmea wa kahawa ambao utaweza kustahumili ukame na pia unanuia kuundwa kwa Bodi ya kahawa ya Kenya.
Mkutano huu na wakulima wa kahawa katika Kaunti ya Kiambu ulizua tumbo joto baina ya wakulima, madalali na maofisa wa vyama vya ushirika.
Wakulima wakiwalaani vikali madalali na maofisa wa vyama vya ushirika wakidai kuwa wao wanawadhulumu kama wakulima wa kahawa wanaofanya kazi ya mchwa kukuza kahawa.
Wakulima wa kahawa wanapitia hali ngumu ya kulima, kupalilia na kuvuna kahawa.
Lakini ukiwadia wakati wa kuuza, madalali na maofisa wa vyama vya ushirika wanavuna wasipopanda na kufaidika kiulaghai ilhali mkulima anaendelea kunyanyaswa.
Wakulima waliomba kuhusishwa bila kupitia kwa madalali katika mauzo yao ya kahawa.
Walikiri wakiondolewa madalali ndipo mkulima wa kahawa ataweza kufaidika na pato la kahawa kama ilivyokuwa hapo awali.
Wanakamati waliwasihi wakulima waongozwe na maadili mema.
Wasilie tu kuhusu ufisadi Ilhali wao ndio wanaokuza ufisadi.
Waliwahakikishia wakulima kuwa wameskia kilio chao, na watafanya juhudi ya kuona Mswada wa kahawa wa mwaka 2021 unapitishwa ili mkulima wa kahawa Nchini anufaike.